Mazungumzo ya simu kati ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakuu wa nchi za kanda hii ni duru mpya ya mashauriano ya kidplomasia inayofanya Tehran kwa shabaha ya kuzidisha mashirikiano ya kikanda. Mashauriano aliyofanya Rais wa Iran yanaonyesha kuwa nchi jirani zina nafasi maalumu katika sera za nje za Iran.
Pezeshkian amezungumza kwa simu na Sheikh Muhammad bin Zaid Al Nahyan Rais wa serikali ya Imarati (UAE) na akasema: Iran inataka kuimarisha zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla uhusiano wake jirani na za Kiislamu na inakaribisha suala la kupanua ushirikiano kati ya pande mbili.
Kwa upande wake, Rais wa serikali ya Imarati amesema katika mazungumzo hayo ya simu: "nina hamu kubwa ya kuitembelea Iran haraka iwezekanavyo, ili kwa pamoja tuweze kusaidiana katika kuasisi na kuimarisha madaraja ya mawasiliano kati ya nchi zetu mbili kwa kuzingatia maslahi ya pamoja na mustakbali mwema wa mataifa yetu".
Rais wa Iran alizungumza kwa simu pia na Amir wa Kuwait Mishal al Ahmad al Jaber al Sabah na kusema:" Tuko tayari kwa ushirikiano wa aina yoyote ili kupanua mahusiano katika nyanja mbalimbali na Kuwait na majirani wengine ili kuimarisha uhusiano wa kidugu na ujirani mwema."
Amir wa Kuwait kwa upande wake amesema kuwa: Kuwait inataka kupanua zaidi ya hapo kabla uhusiano wake na Iran, na kuhusiana na hili inakaribisha jumbe na mielekeo chanya na athirifu katika kuimarisha uhusiano na nchi jirani na rafiki.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza kwa njia ya simu pia na Mfalme Abdallah bin Hussein wa Jordan, Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa wa Bahrain na Waziri Mkuu wa Iraq Muhammad Shia al Sudani.
Katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq, Dakta Pezeshkian amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapenda kupanua uhusiano na nchi rafiki, ndugu na jirani yake wa siku nyingi katika nyanja mbalimbali.
Katika mazungumzo hayo, naye Waziri Mkuu wa Iraq amesema: "Ninatumai kwamba juhudi zinazofanywa zitapelekea kuongezeka umoja na mshikamano na kuimarishwa udugu baina ya Iran na Iraq na nchi zote za Kiislamu; na kupitia umoja huo tutaweza kustawisha zaidi na zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi za Kiislamu".
Muelekeo ulioonyeshwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya karibuni umekuwa kigezo chema na athirifu cha kuongezeka ushirikiano baina yake na nchi jirani; ambapo leo hii aghalabu ya nchi za kanda hii zinafuata mwenendo huu wa diplomasia yenye mafanikio.
Iran ambayo ni nchi yenye uwezo na fursa za aina kwa aina katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii pamoja na rasilimali watu yenye uwezo mkubwa, itakuwa na nafasi nzuri na athirifu katika kutoa mchango wa kuboresha mshikamano na mashirikiano yenye wigo mpana kati yake na nchi jirani.
342/
Your Comment